Watu watatu wa familia moja wamefariki dunia baada ya nyumba kuteketea kwa moto Mtaa wa Nyarusrya, Manispaa ya Musoma, Mkoa wa Mara.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kuwa chanzo cha moto huo kinachunguzwa.
Moto huo ambao chanzo chake bado hakijajulikana umepelekea kifo cha mtumishi wa Wizara ya Maji, Rochi Mkolekuwa (39), aliyekuwa Meneja wa Ubora wa Maji katika Maabara ya Mkoa wa Mara, Mariam Msigwa (34) na mtoto wao, Rochi Shaban (4).
Magere amesema walipata taarifa ya tukio hilo saa 10 usiku wa kuamkia leo Jumatatu Januari 5, 2026 na walipofika katika nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi walikuta imeteketea na watu hao wakiwa ndani.
Amebainisha kuwa taarifa ya tukio hilo ilichelewa kutolewa walipofika eneo la tukio waliwakuta wakiwa tayari wamefariki dunia ambapo mwili wa baba ulikutwa sebuleni huku miili ya mama na mtoto ikiwa chumbani.

