Ijumaa , 27th Feb , 2026

Chama cha Waganga wa Tiba Asilia na Wakunga wa Jadi (CHAWATIATA) imeanza msako mkali wa kuhakiki na kuwaondoa waganga feki jijini Tanga wanaotuhumiwa kwa vitendo vya udhalilishaji na ukiukwaji wa maadili kwa kisingizio cha kutoa tiba za kienyeji. Hatua hiyo inalenga kulinda heshima ya taal

Chama cha Waganga wa Tiba Asilia na Wakunga wa Jadi (CHAWATIATA) imeanza msako mkali wa kuhakiki na kuwaondoa waganga feki jijini Tanga wanaotuhumiwa kwa vitendo vya udhalilishaji na ukiukwaji wa maadili kwa kisingizio cha kutoa tiba za kienyeji. Hatua hiyo inalenga kulinda heshima ya taaluma ya tiba asili na kuhakikisha usalama wa wananchi.

Baadhi ya waganga wa tiba asilia jijini Tanga wametuhumiwa kujihusisha na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake kwa kisingizio cha kuwatoa nuksi na kuwasafisha nyota.

Tuhuma hizo zimeeleza kuwa vitendo hivyo hufanyika kwa madai ya kukamilisha tiba za kienyeji. Hali hiyo imezua hofu na mjadala mkubwa katika jamii.

Inadaiwa kuwa baadhi yao wanawaogesha wanawake wakiwa wamewavalisha nguo zisizositiri maumbile yao jambo linaloonekana ni kinyume na taratibu zinazoongoza huduma ya tiba asili.

Baada ya hatua hiyo, hutokea vitendo vya ukatili wa kijinsia wakidai ni sehemu ya matibabu.

Matukio hayo yamelalamikiwa na wananchi wakiwemo waganga wa tiba asili wakitaka hatua kali zichukuliwe kulinda heshima ya taaluma hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Chama cha Waganga wa Tiba Asilia na Wakunga wa Jadi (CHAWATIATA) kimeanza zoezi la kuhakiki upya usajili wa waganga wa tiba asili jijini Tanga.

Zoezi hilo linalenga kubaini waganga wasio na sifa na kuwaondoa rasmi hatua hiyo inalenga kulinda hadhi ya taaluma ya tiba asilia.

Akizungumza na EATV, mjumbe wa CHAWATIATA mkoa wa Tanga, Ibrahimu Ikungo, alisema baadhi ya wanaojiita waganga hawajasimikwa kwa kufuata taratibu za mila.

Alisema usimikaji hufanywa na wazee wenye mamlaka ya jadi Bila hatua hiyo, mtu hawezi kuitwa mganga halali.

“Mganga halali lazima asimikwe na apewe maelekezo rasmi, vinginevyo huyo ni tapeli,” alisema Ikungo. Aliongeza kuwa wapo watu wanaojifunza kwa muda mfupi kisha kuanzisha huduma zao. Tabia hiyo imekuwa chanzo cha malalamiko mengi,”amesema Ikungo.