Jumatano , 25th Mei , 2022

Kufuatia changamoto kadhaa zilizotajwa kuwepo katika soko la kimataifa la samaki feri Jijini Dar es Salaam Katibu Mwenezi wa Chama Cha mapinduzi CCM Shaka Hamdu Shaka, ametoa siku saba kwa pande mbili za serikali na wafanyabiashara kukaa na kuzipatia ufumbuzi.

Soko la Feri

Hili soko la samaki feri linatajwa kama soko la kimataifa likiuza samaki wa aina mbalimbali ambapo licha ya umahiri wake zipo changamoto kadhaa.

"Sisi hapa kwenye hili soko ukishusha samaki hata kabla hujauza unaambiwa ulipie ushuru na ushuru ni mkubwa hali inayotufanya kuyumba kweli kweli" amesema Hamadai Kombo mmoja ya wafanyabiashara soko la feri

Kufuatia kero zilizowasilishwa ikamlazimu Mkurugenzi wa Jiji La Dar es Shauri Jumanne Shauri kutoa majibu huku viongozi wa soko hilo wakieleza hatua ambazo kama soko wamekwishachukua.

"Kuna sheria ndogo ziliundwa ili kufanya mabadiliko ya kiutendaji sokoni hapo kutoa baadhi ya viongozi kwa ngazi ya jiji ili uwajibikaji uwepo changamoto zingine tumezipokea kwa utekelezaji"amesema Jumanne Shauri, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.

Wakati hayo yakijiri katibu wa itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Shaka Hamdu Shaka, akawataka viongozi kuacha kufanya kazi kwa mazoea huku akikiri uwepo wa changamoto hizo na kuwasisitiza viongozi pande zote kuzitatua.