Alhamisi , 26th Jan , 2023

Kukosekana kwa uzio pamoja na wanafunzi, kutembea umbali mrefu katika maeneo yanayozingirwa na vichaka zimetajwa kuwa changamoto zinazochangia kuongezeka kwa matukio ya ukatili yakiwemo ulawiti na ubakaji kwa baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi katika kata ya Goba wilayani Ubungo Dar

Hayo yamebainishwa katika shule mbili za msingi Kunguru na Kulangwa zilizopo mtaa wa Tegeta "B" katika kata ya Goba baada ya wanafunzi pamoja na walimu wa shule hizo kueleza kutofurahishwa mazingira wanayokutana nayo wanafunzi wakiwa shuleni na hata wakati wa kurejea majumbani kutokana na maeneo mengi kuzungukwa na mapori ambayo yamekua yakihatarisha usalama wao.

Licha ya wanafunzi wa shule hizo kuwa kwenye hatari ya kukumbwa na matukio ya ukatili lakini pia shule inakabiliwa na upungufu wa madawati, viti pamoja na meza za walimu hali inayowalazimu baadhi ya walimu kutumia madawati ya wanafunzi wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Kufuatia changamoto zinazoikabili shule hizo baadhi ya viongozi kutoka jumuiya ya wazazi ya chama cha mapinduzi CCM kata ya Goba wakatembelea katika shule hizo lengo likiwa ni kuangalia namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wa shule hizo.