Jumatano , 31st Dec , 2025

Katika chapisho lake, Trump ameendeleza ukosoaji mkali dhidi ya familia hiyo maarufu ya kisiasa, kauli iliyozua ghadhabu na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wananchi na wachambuzi wa siasa, wengi wakisema hatua hiyo haikuwa na maadili wala heshima.

Muda mchache baada ya kifo cha Mwandishi wa habari za mazingira, Tatiana Schlossberg, binti wa mwanadiplomasia wa zamani Caroline Kennedy na mjukuu wa aliyekuwa Rais wa Marekani John F. Kennedy, ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 35, Rais wa Marekani Donald Trump ameishambulia familia ya Kennedy kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.

Familia ya Schlossberg imechapisha taarifa za kifo chake kwenye akaunti za mitandao ya kijamii za JFK Library Foundation jana Jumanne Disemba 30 ikisema Tatiana amefariki dunia asubuhi na kuongeza kuwa ataendelea kuishi mioyoni mwao milele.

Kifo chake kimekuja siku chache tu baada ya kufichua ugonjwa wake mwezi Novemba, akieleza kuwa aligunduliwa na acute myeloid leukemia, aina adimu na kali ya saratani ya damu isiyotibika ambayo mara nyingi huwapata watu walio na umri wa zaidi ya miaka 60.

Katika chapisho lake, Trump ameendeleza ukosoaji mkali dhidi ya familia hiyo maarufu ya kisiasa, kauli iliyozua ghadhabu na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wananchi na wachambuzi wa siasa, wengi wakisema hatua hiyo haikuwa na maadili wala heshima, hasa ikizingatiwa kuwa familia hiyo bado katika kipindi cha maombolezo.

Donald Trump hakukitaja moja kwa moja kifo cha Tatiana Schlossberg katika msururu wa machapisho aliyoyaweka kwenye mitandao ya kijamii baada ya kifo chake. Badala yake, amechapisha picha za wafuasi wake wa MAGA wakiidhihaki familia ya Kennedy, kufuatia kauli zao za hivi karibuni kupinga uamuzi wake wa kuongeza jina lake katika Kennedy Center.

Kennedy Center ni ukumbi wa kihistoria wa maonyesho uliopo Washington, D.C., ambao ulitengwa rasmi kama kumbukumbu ya Rais John F. Kennedy baada ya kuuawa kwa kupigwa risasi mjini Dallas, Texas, mwaka 1963.

Katika taaluma yake, Schlossberg aliandika kwa upana katika machapisho makubwa yakiwemo The Atlantic na Vanity Fair. Mwaka 2019, alichapisha kitabu kilichoshinda tuzo kiitwacho “Inconspicuous Consumption: The Environmental Impact You Don't Know You Have,” kinachochambua athari za mazingira zisizotambuliwa kwa urahisi katika maisha ya kila siku.

Tatiana ameacha nyuma mume wake, George Moran, pamoja na watoto wao wawili.