
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na Balozi wa China nchini Balozi Wang Ke.
Balozi Ibuge katika kikao hicho na Balozi Wang Ke, amesisitiza msimamo wa Tanzania kuunga mkono nia ya Bara la Afrika kuwa na nafasi mbili za uwakilishi wa kudumu katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Amefafanua kuwa, Nchi za Afrika zinataka uwakilishi huo uwe na nguvu ikiwa ni pamoja na kupata nafasi moja ya kura ya Veto kama walivyokubaliana katika mkutano wa Ezulwini na Azimio la Sirte la mwaka 1999.
Balozi Ibuge pia amezungumzia kuhusu utekelezzaji wa mambo maalum ambayo yamo katika Hotuba ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa kuzindua Bunge la 12, tarehe 13 Novemba 2020 jijini Dodoma, ambapo amemuomba Balozi Wang Ke kufikisha mambo yaliyomo katika hotuba hiyo kwa wawekezaji wa China ili kuwekeza nchini.
Balozi Ibuge amesema maono ya Mhe. Rais aliyoyasema katika hotuba yake ni utekelezaji wa moja ya kauli iliyowahi kutolewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa "wakati wengine wanatembea Watanzania tunatakiwa tukimbie." ili kufikia maendeleo kwa haraka.
Kwa Upande wake Balozi Wang Ke amemuhakikishia Balozi Ibuge, kwamba China iko pamoja na Bara la Afrika na kwamba wanaunga mkono mapendekezo ya Bara la Afrika ya kuwa nafasi mbili za kudumu katika Baraza hilo.
Balozi Wang Ke ameelezea kufurahishwa na maono ya Mhe. Rais yaliyobainishwa katika Hotuba hiyo na kuahidi kuendelea kuisaidia Tanzania ili kufakisha maono hayo kwa vitendo na kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo.
Viongozi hao pia wamejadiliana na kubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kindugu baina ya Tanzania na China kwa faida ya pande zote mbili.