Jumatatu , 8th Sep , 2025

Aliyekuwa daktari wa nusukaputi amefikishwa mahakamani katika mji wa Besançon, mashariki mwa Ufaransa, akituhumiwa kuwapata sumu kwa makusudi watu 30, wakiwemo wagonjwa 12 waliofariki.

Frédéric Péchier, 53, aliwekwa chini ya uchunguzi miaka minane iliyopita, aliposhukiwa kuwapa wagonjwa sumu katika kliniki mbili za jiji kati ya 2008 na 2017

Licha ya mashtaka mazito dhidi yake, Péchier amesalia huru chini ya uangalizi wa mahakama na aliiambia redio ya Ufaransa Jumatatu "hakuna uthibitisho wa sumu yoyote."

Kesi hiyo inatarajiwa kudumu kwa zaidi ya miezi mitatu na inahusisha zaidi ya raia 150 wanaowakilisha waathiriwa 30.

Madai ya sumu yaliibuka Januari 2017, wakati mgonjwa mwenye umri wa miaka 36 anayeitwa Sandra Simard, aliyekuwa mzima wa afya, alipofanyiwa upasuaji kwenye mgongo wake na moyo wake ukaacha kupiga.

Baada ya daktari wa wagonjwa mahututi kushindwa kuuamsha moyo, Frédéric Péchier alimdunga sindano na mgonjwa huyo alipata koma na baadaye kuamka. Dawa aliyotumia kumdunga ilionyesha kiwango cha potasiamu mara 100 ya kipimo kilichotarajiwa.

Mmoja wa mawakili wa Péchier amesema yuko tayari kuthibitisha kuwa hana hatia, na daktari huyo wa zamani ameiambia redio ya RTL Jumatatu kwamba ni fursa ya kuweka mambo sawa.

Kesi kumi na mbili za kutiliwa shaka zinazohusisha wagonjwa ambao hawakuweza kuamka zinamkabili.
Damien Iehlen alifariki Oktoba 2008. Akiwa na umri wa miaka 53 alikwenda katika Kliniki ya Saint-Vincent ambako mtuhimiwa alikuwa akifanya kazi, kwa ajili ya upasuaji wa kawaida wa figo na alifariki baada ya mshtuko wa moyo. Uchunguzi ulionyesha alikuwa amepewa kiwango kikubwa cha dawa ya lidocaine.

Frédéric Péchier anatoka katika familia ya wataalamu wa afya; baba yake pia alikuwa daktari wa ganzi.
Kesi hiyo imepangwa kuendelea hadi Desemba na mshtakiwa ataendelea kuwa huru, chini ya uangalizi wa mahakama. Ikiwa atapatikana na hatia atakabiliwa na kifungo cha maisha.