Jumanne , 16th Mar , 2021

Daraja linalounganisha Tarafa za Bulambya na Undali, lililopo wilaya ya Ileje mkoani Songwe, limezidi kuzua taharuki baada ya kujengwa na kudondoka kwa mara ya pili mfululizo hali iliyopelekea wananchi kukosa mawasiliano kwa Tarafa zote mbili.

Daraja lililobomoka

Daraja hilo ambalo lilikarabatiwa na kukamilika jioni ya Machi 14, 2021, na ilipofika majira ya usiku daraja hilo likaanguka tena ambapo hadi sasa uongozi wa serikali umeendelea na taratibu za kujenga kivuko cha muda ambacho kitaondoa kero za wananchi wa tarafa hizo.

Wananchi wa Kata hizo wamedai kuwa daraja hilo ni mkombozi kwao hivyo tangu kuvunjika kwa daraja hilo imekuwa ni vigumu kwao katika nyanja ya kibiashara lakini pia wanafunzi wa shule za msingi wengi wamekwama kuendelea na masomo kutokana na daraja hilo kuvunjika.

Hali imezidi kuwa tete kwa upande wa usafiri kwani kutokana na daraja hilo kuanguka, sasa kumejitokeza biashara ya vijana kuvusha watu na pikipiki kwa kiasi cha shilingi 2,000 hali ambayo haikuzoeleka na wananchi.

Pamoja na jitihada za kujenga kivuko cha muda, wananchi wamedai kuwa kama kutakuwa na mvua katika kipindi hiki huenda kivuko hicho kikaondolewa na maji kwani si cha uhakika na kuiomba serikali kuwatengenezea daraja la uhakika ili mawasiliano katika Tarafa hizo mbili yaweze kurejea.