Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya mkoani Mtwara imefanikiwa kuteketeza kilo 73 za dawa za kulevya aina ya bangi, baada ya kesi zake kukamilika mahakamani na mahakama kutoa uamuzi wa kuziteketeza.
Akizungumza wakati wa zoezi la kuteketeza dawa hizo zilizokamatwa mkoani humo, Afisa Sheria wa mamlaka hiyo Kanda ya Kusini, Jagadi Jilala, amesema zoezi hilo limefanyika kwa uwazi, kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali.
“Zoezi hili linafanyika ili kuhakikisha dawa za kulevya zilizokamatwa, na mashauri yake yamesikilizwa mahakamani na maamuzi ya kuteketeza yamekubaliwa, hazirudi mitaani kuathiri jamii,” amesema Jilala.
Kufuatia tukio hilo, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya mkoani Mtwara imetoa wito kwa jamii kutojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, kutokana na madhara yake makubwa kiafya na kijamii, hasa kwa vijana.

