Jumanne , 22nd Jan , 2019

Mkuu Wa Wilaya ya Masasi Mh. Ramadhani Mzee, ametoa maelezo juu ya picha inayozunguka mitandaoni ikionesha choo cha nyasi kinachotumiwa na wajawazito katika zahanati ya Namalembo, wilayani humo.

Picha ya choo kilichozua mjadala

Akizungumza na www.eatv.TV, Mh Mzee amesema kwamba picha hiyo ni ya zamani sana na kwamba serikali ilishafanya jitihada za kutengeneza choo bora na cha kisasa katika zahanati hiyo.

"Hiyo picha ni ya zamani Kama miaka miwili iliyopita, sasa hivi kimeshajengwa choo cha kisasa na muda si mrefu kitaanza tumika. Sijui hao wanaosambaza hiyo picha sasa wanalenga nini, ila ni picha ya miaka miwili nyuma", amesema DC Mzee.

Picha hiyo ambayo iliyopakiwa na baadhi ya watu mitandaoni, imeibua mijadala hasa kwa baadhi ya wabunge wa upinzani, akiwemo Mbunge Wa Tarime, John Heche ambaye alisambaza ujumbe huo katika ukurasa wake wa Twitter.

Picha hiyo ilisambazwa kwa mara ya kwanza na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Kumbusho Dawson katika ukurasa wake wa Twitter na kuzua mjadala mkubwa juu ya ubora wa huduma za afya hasa maeneo ya vijijini.