Jumamosi , 10th Dec , 2022

Mkuu wa wilaya ya Magu Salum Kalli amewaonya wakazi wa wilaya hiyo kuacha kuendekeza mila potofu zinazochangia ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia na kusema hatua za kisheria zitachukuwa dhidi ya watakaokaidi agizo hilo

Mkuu wa wilaya huyo ametoa kauli hiyo leo hii wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili ambapo amesema hivi karibuni katika kijiji cha Nyang'anga kata ya Sukuma wilayani humo baadhi ya wanawake walipewa adhabu ya kuchimba kaburi wakituhumiwa kusababisha mauaji ya vijana katika kijiji hicho

"Mila potofu kwa kina mama na watoto ambazo huchangia ongezeko la vitendo vya ukatili nawaomba tuziache mara moja serikali inatoa maelekezo kila kukicha lakini kwanini bado mnaziendekeza? kama ile ya wanawake kuchimbishwa kaburi katika wilaya hii iwe mwanzo na mwisho sitakubali jambo hilo hata dini zetu haziruhusu naomba muache mara moja"

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya akakemea wazazi wanaowatumikisha watoto wao kwa kuwapa bishara wauze mitaani 

"Marufuku mtoti yoyote kuonekana sehemu za biashara au mitaani anauza sijui karanga au mahindi na pia nawaomba tuwachunge watoto wetu wasifanyiwe vitendo vya ukatili na ikitokea amefanyiwa basi tutoe taarifa hata kama aliyefanya ni ndugu wa karibu"

Kwa upande wake kaimu afisa ustawi wa halmashari ya wilaya ya Magu KMercy Lemge amesema kwa kipindi cha kuanzia mwezi July 2021 hadi kufikia June 2022 matukio ya ukatili yaliyoripotiwa yalikuwa 635 huku mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la KIVULINI Yassin Ally akiiomba mahakama iharakishe kutoa maamuzi ya mashauri ya ukatili wa kijinsia endapo ushahidi ukikamilika mapema