Jumanne , 28th Mar , 2023

Watu wawili ambao hawajajulikana hadi sasa wamemshambulia na kumsababishia kifo kijana mmoja anayefahamika kwa jina la Zulkif Hemedi ambaye ni dereva bodaboda mkoani Lindi

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoani Lindi  Pili Mande amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo ambapo amesema vijana hao wawili walimhadaa dereva bodaboda huyo na mwishowe kumjeruhi kwa kitu chenye ncha kali na kumsababishia kifo

Taarifa za wananchi na viongozi katika kijiji cha Nangaru zinasema, Bodaboda huyo ambaye kwa asili ni mzaliwa wa Kijiji cha Nangaru, alifuatana na abiria hao wawili ambao alielekea nao upande wa mashambani, lakini baada ya mda mfupi alifanikiwa kuwapigia simu rafiki zake aliowasabahi kijiweni na kuwataarifu kuwa, abiria wake wamemgeuka na kumshambulia vibaya kiasi cha kupoteza fahamu.

Inasemekana kuwa, walipomshambulia na kumwacha chini, walifanikiwa kumpora simu kubwa na kumwacha marehemu na simu ndogo ambayo hawakufahamu kama aliificha mfukoni. 

Baada ya kupiga simu na kuomba msaada, wasafirishaji wenzake walitoa taarifa kijijini na kufanya msako mkubwa hadi kijiji jirani ambapo  walifanikiwa kuzuia barabara lakini jitihada za kuwakamata wahalifu hao iligonga ukuta, kwani walifahamu njama ya wanakijiji na kuamua kuitelekeza pikipiki vichakani na kukimbia.

Jeshi la Polisi Mkoani Lindi linaendelea kufanya msako mkubwa ili kuwabaini wahalifu hao huku polisi wakiwataka Madereva bodaboda wote kuwa na umoja lakini pia kusoma alama za hatari mapema ili waweze kujilinda na kutoa taarifa wanapohisi wapo mashakani