Ijumaa , 21st Nov , 2025

"Ninaelekeza Kamishna wa uhamiaji kamata passport yake asitoke nje ya nchi mpaka jambo hili liishe tumemwajiri tumemlipa anajiamlia kama aje kwenye mradi ama asije huyu ni mhalifu akamatwe na asitoke nje ya nchi mpaka jambo hili liishe,"

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba amemuagiza Kamishna wa Uhamiaji na Mkuu wa jeshi la polisi nchini kumkamata na kuzuia hati ya kusafiria (passport) ya mkandarasi aliyekuwa akijenga mradi wa kituo cha pamoja cha ukaguzi wa magari kilichopo kata ya Muhalala Wilayani Manyoni Mkoani Singida kwa kushindwa kukamilisha mradi huo na kuutelekeza kwa zaidi ya miaka nane.

Dkt. Mwigulu amesema hayo leo Novemba 21 alipokuwa akizungumza na wananchi mara baada ya kuwasili Mkoani Singida ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhfa huo.

Amesema mkandarasi aliandikiwa barua kufika katika eneo la mradi huo siku tano zilizopita lakini ameonesha dharau ya kutokufika huku akijua wazi kuwa ameiletea hasara serikali.

Mradi huo ulianza kujengwa mwaka 2016 na ulitakiwa kukamilika mwaka 2017 lakini ulisimama tangu mwaka 2018 huku ikielezwa kuwa mkandarasi alidai kufilisika huku kesi ikipelekwa nchini kwao Italia na kutakiwa kuilipa Tanzania.

"Kulikuwa na majadiliano yanaendelea ya kisera kati ya mkandarasi na serikali, serikali ikatatua ule mkwamo ulikuwepo, kwataarifa sahihi nilizonazo mkandarasi akatangwa kwa amefilisika kule kwao wa kutoka Italia, akatangaza amefilisika hawezi kuendelea na mradi mahakama ya kule ikaelekeza mkandarasi yule ailipe Tanzania kwasababu aeicheleweshea huu mradi, nikasikia zikaanza ngonjera," amesema.

Nimepita pale nikauliza yupo wapi mkandarasi nimeambiwa wakandarasi wasaidizi wapo nilikuwa namsikiliza wakandarasi wasaidizi kwamba hakuweza kufika kwasababu ya ratiba, lakini nimeelekeza siku karibu tani nikisema mkandarasi pamoja na sekta waje hapa kwenye eneo la mradi kwenye la tukio ambao umekwama kwa muda mrefu unatia aibu nchi yetu, moja alijua amefilisika hajutaka kuachia mradi hajataka wakandarasi wazawa waendelee na mradi amefilisika ameng'ang'ania mradi amending barua hajaja huku ni kuwahujumu vijana wa kitanzania ambao wangepata kazi hapa huku ni kuhujumu uchumi wetu.

Sasa ninaelekeza Kamishna wa uhamiaji kamata passport yake asitoke nje ya nchi mpaka jambo hili liishe tumemwajiri tumemlipa anajiamlia kama aje kwenye mradi ama asije huyu ni mhalifu akamatwe na asitoke nje ya nchi mpaka jambo hili liishe," ameongeza Dkt. Mwigulu.

Dkt. Mwigulu ameagiza mradi huo kuhamia Wizara ya Ujenzi kutoka wizara ya fedha huku akisema kuwa ni wakati sasa wa kuanza kuwaamini wakandarasi wazawa.