Alhamisi , 22nd Apr , 2021

Mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 15, mwanafunzi wa shule ya sekondari Kwang iliyopo Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara ambaye jina lake limehifadhiwa amebakwa na dereva pikipiki maarufu kama bodaboda majira ya asubuhi wakati akienda shule kisha dereva huyo kukimbia.

Kamanda wa Polisi Manyara Paul Kasabago

Akisimulia tukio hilo Kamanda wa Polisi Manyara Paul Kasabago amesema kuwa majira ya asubuhi wanafunzi wawili wa kidato cha tatu wanaoishi Mtaa wa Sinai uliopo kata ya Maisaka wakiwa wanakwenda shule alitokea dereva pikipiki anayefahamika kwa jina la Paskal Fisoo mkazi wa kijiji cha Soraa ambaye alisimama mbele yao na kuwaomba kuwapa lifti ili waweze kufika shuleni mapema.

“Wasichana hao wakakubali wakapanda lifti hiyo badala ya kuwapeleka shuleni yeye akakata kona, akaingia mkono wa kulia machakani na alipofika umbali kama wa kilomita moja, akachomoa sime na kuwatisha, mwanafunzi mmoja alitoroka, mmoja akawa ndiye ametekwa na akabakwa, aliyetoroka akaenda moja kwa moja stendi na kutoa taarifa polisi, hadi sasa pikipiki hiyo tunayo mtuhumiwa tunaendelea kumtafuta,” amesema Kamanda Kasabago.

Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Mji wa Babati Frank Mchuno amethibitisha kumpokea mwanafunzi huyo na kumkuta na majeraha mengi kwenye mwili wake ikiwemo sehemu za siri na kisha kumpatia dawa za kuzuia maambukizi.

Kamanda wa Polisi Kasabago akatumia nafasi hiyo kuwaonya vijana waache tamaa za mwili zitawatia hatiani na kuishia kutumikia kifungo cha jela miaka thelathini au kifungo cha maisha.