Jumanne , 20th Apr , 2021

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk. Edward Hoseah amesema suala la Katiba mpya ni kilo cha chama hicho huku akiahidi kukaa pamoja na serikali kuona ni kwa namna gani wanalifanyia kazi suala hilo endapo watapata nafasi hiyo.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk. Edward Hoseah

Dk. Hoseah amesema hayo leo katika mahojiano kwenye kipindi cha Supa Breakfast ambapo amesema akipata nafasi ya kuzungumza na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan atazungumzia kuhusiana na suala la Katiba kwani lipo katika moja ya ajenda zake.

"Kilio chetu kama Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ni kutazama hii rasimu ya Katiba na tunao wataalum wa Katiba, tukae na serikali tuone ni kwa namna gani suala zima la Katiba mpya tunalitazama, ni jambo linalonisukuma," amesema Dk. Hoseah.
 
Pia Dk. Hoseah amesema kuwa upo umuhimu wa kuzingatia utwala bora wa sheria nchini huku akieleza kuwa kuna sheria zinatakiwa zifanyiwe marekebisho hususani katika suala la dhamana kwani mfumo wa haki jinai ni mfumo shindanishi na sheria zilizopo kwenye suala la dhamana hakuna usawa kwa watu wote.

Awali akizungumzia uteekelezaji wa ajenda zake ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wake na endapo atahitaji kuongezewa muda, Dk. Hoseah amesema mwaka mmoa unamtosha kutekeleza yale yote aliyoahidi.

"Katika suala la uongozi, kiongozi usitake uongezewe muda, kama wanaTLS wataona uongozi wangu umefanya kazi nzuri na wakaridhia tuendelee sawa lakini sisi hatutadai hata sekunde, mwaka mmoja kwa yale niliyoyaahidi nitatekeleze,"amesema Dk. Hoseah.