
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, ameahidi kuendelea kutumbua majipu na kuwaagiza wakuu wa mikoa nchini, kuhakikisha wananchi wao hawakumbwi na njaa na atakayeacha wananchi wakakosa chakula na kupoteza maisha atawajibishwa mara moja.
Dk. Magufuli ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu leo alikuwa amevalia kombati za kijeshi ameyasema hayo Jijini Arusha, wakati akiwa njiani kuelekea kwenye zoezi la kijeshi wilayani Monduli, katika hitimisho la zoezi la Onesha Uwezo wa Medani, Brigedia 303, ambapo akiwa njiani alilazimika kusimama maeneo mbalimbali, kuzungumza na wananchi waliokuwa wamefurika pembeni mwa barabara kumlaki.
Amesema yeye kama Rais wa nchi hawezi kukubali kuona wananchi wanakufa kwa njaa na endapo mwananchi akifa kwa njaa, mkuu wa mkoa husika atawajibika bila ya kupepesa macho na kuchelewa.
Huku akishangiliwa na wananchi Dk. Magufuli pia amesema ataendelea kutumbua majipu yanayonuka, yasiyoiva na vipele vidogovidogo, vinavyoota kwani ndani ya vyama mbalimbali vya siasa, hata ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) napo kuna majipu yanayohitaji kutumbuliwa.