Jumatatu , 15th Sep , 2014

Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi, ni miongoni mwa wafanyabiashara wanne waliofikia fainali ya kuwania Tuzo ya Mwaka ya Mfanyabiashara Bora Afrika (AABLA) kundi la Afrika Mashariki.

Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Dkt Reginald Mengi.

Taarifa iliyopatikana jijini Dar es Salaam inaeleza kuwa sherehe za tuzo za AABLA, kundi la Afrika Mashariki zitafanyika Septemba 20 mwaka huu jijini Nairobi na kurushwa moja kwa moja hewani na luninga kadhaa barani Afrika.

Kwa mujibu ya chaneli ya televisheni ya masuala ya fedha na biashara Afrika (CNBC Africa), ambao ndio waandaji wa sherehe hizo, tuzo za AABLA zimebuniwa kwa ajili ya kutambua utendaji uliotukuka katika biashara, wenye mafanikio makubwa kwenye sekta zao za biashara na vilevile kwenye jamii ambapo biashara hizo zinaendeshwa.

 “Tuzo hizo ni kutambua uongozi wa watu hao katika kubadilisha sekta ya biashara kwa kuendeleza ubora wa shughuli zao kwa kuzingatia desturi njema za kufanyabiashara na ubunifu.”

“CNBC Africa inajivunia kuendeleza utamaduni uliowekwa na tuzo hizi unaotambua na kusherekea mtazamo, msukumo wa mafanikio na ubora mkubwa wa viongozi wafanyabiashara katika bara la Afrika. AABLA iinawatambua kipekee na kuwaheshimu  viongozi  ambao wamechangia katika kuboresha uchumi wa Afrika na wamiliki wa biashara zinazoongoza wakati huu," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Washindi wa tuzo hizi ni mfano mzuri zaidi katika uongozi Afrika. Wao ni uthibitisho wa thamani halisi wa kiongozi aliyefanyikiwa, - mafanikio,- nguvu, ubunifu, -ustadi, -ujuzi na –uwezo wa kuona mbali – thamaini amabazo ni muhimu katika kuunda biashara kubwa katika uchumi wa Afrika na ulimwengu,”  kama ilivyoandikwa katika tovuti : https://www.aabla2014.com.

AABLA ni tuzo moja kubwa zaidi ya biashara barani Afrika na hutolewa katika kanda za Afrika Magharibi, Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Wafanyabiashara wengine watatu wateule wa tuzo hiyo ni Ofisa Mtendaji wa BRITAM, Benson Wairegi, (Kenya), Ofisa Mtendaji wa CENTUM, James Mworia, (Kenya) na Ofisa Mtendaji  wa CROWN PAINTS, Rakesh Rao (Kenya).

Watanzania wengine walioteuliwa katika tuzo hizo kwa makundi tofauti ni Ofisa Mtendaji wa Helvetic Solar Ltd, Patrick Ngowi, (EA Young Business Leader) na Ofisa Mtendaji wa Techno Brain Ltd, Manoj Shanker, (Entrepreneur of the Year).