Jumatano , 18th Aug , 2021

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametuma salamu kwa watendaji wa Mtaa wa Ghana Mkoani Mwanza ambapo anaishi mtoto aliyekoseshwa haki ya kwenda shule ili abaki nyumbani akimuuguza Bibi yake wakati watendaji wapo katika eneo hilo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima

Hii inafuatiwa baada ya kuripotiwa kwa vyombo vya habari juu ya  mtoto huyo anayefahamika kwa jina la  Shamsa Ramadhani mwenye umri wa miaka tisa ambaye amebeba jukumu la kumuuguza bibi yake kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ilihali baba yake yuko hai na hajawahi kumuona.

“Pale Mwanza naenda huko kesho kutwa mtoto ameachishwa shule ana miaka 9 anamuuguza bibi yake eti system haijui wanafanya nini pale kama wewe ni kiongozi huna mbinu za kusikiliza taarifa ya habari, kusoma taarifa mbalimbali wewe ni tatizo, Mwanza mwambieni, Mtendaji wa Mtaa, Kata, ambayo yupo mtoto aliyenyimwa haki ya kwenda shule, ana miaka tisa pamoja na akili yote hiyo haendi shuleni watendaji wametulia tulia wanasubiri ndugu wajitokeze nakuja Mwanza," alisisitiza Waziri Dkt. Gwajima.

Pia Dkt. Gwajima alieleza kuwa katika baadhi ya maeneo nchini watoto wanafanyiwa vitendo vya kikatili na kukoseshwa haki ya elimu ilhali watumishi wanaopaswa kuingilia kati suala hilo wanabaki kimya na kuongeza kuwa baadhi ya watendaji katika ngazi mbalimbali wanabweteka na kulipwa mshahara bila kuufanyia kazi.