Jumapili , 11th Dec , 2022

Jumla ya wafungwa 101 nchini wameachiwa huru Jana Desemba 10, 2022, kufuatia msamaha uliotolewa na Rais Dkt.Samia ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

Rais Dkt Samia kwa ujumla wake ametoa msamaha kwa wafungwa 1,631, ambapo 1,530 kati yao watabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha.

Wafungwa waliopata msamaha huo ni wale wafungwa wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu, wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70, wafungwa walioingia na mimba gerezani, wenye watoto wanaonyonya na wasionyonya.

Wengine ni wale wafungwa wenye matatizo ya akili na wasio na uwezo wa kufanya kazi, wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kuwekwa kuzuizini ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 15 na zaidi na wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani na wametumikia adhabu hiyo kwa miaka 20 au zaidi.

Aidha wenye sifa stahiki wapunguziwe robo ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu, na sharti wawe wamehukumiwa kifungo cha miaka miwili au zaidi ambao wametumikia robo ya adhabu zao gerezani na wawe wameingia gerezani kabla ya Septemba 10 2022.