Jumatano , 28th Apr , 2021

Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbas amesema kuwa vyombo vingi vya habari vinafungwa kutokana na kutokuwa na uwezo wa kimkakati wa kujiendesha kiuchumi.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbas.

Dkt. Hassan Abbas ametoa kauli hiyo wakati akifunga mkutano wa wadau wa habari na kupokea mapendekezo yao kwa ajili ya kuyatolea maamuzi katika kuelekea kilele cha Uhuru wa vyombo vya habari Duniani ambapo amesema kuwa kufungwa kwa vyombo vya habari ni kutokana na sababu za kiuchumi.

Dkt. Abbas ameongeza kuwa mchango wa viongozi Wanawake katika vyombo vya habari umeonekana na kuleta matokeo chanya ikiwemo kuhimiza masuala mazima ya usawa wa kijinsia katika jamii.

"Vyombo vingi vya habari vinafungwa kutokana na kutokuwa na uwezo wa kimkakati wa kujiendesha kiuchumi", amesema Dkt. Abbas.

Kwa upande Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) Rose Reuben akitoa neno kwa niaba ya wadau waliofanikisha mdahalo huo amesema kuwa mafanikio ya sekta ya habari Tanzania yanaonekana na mchango wa Wanawake umeonekana na umezaa matunda.