Dkt. Mengi ataja dawa ya kutibu ulemavu

Jumapili , 17th Mar , 2019

Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP na mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Watu wenye Uhitaji Maalumu (PWDF), Dkt. Reginald Mengi amesema dawa pekee ya kutibu ulemavu ni upendo.

Dkt. Reginald Mengi.

Mengi ameyasema hayo leo Machi 17, 2019 wakati akikabidhi vitabu vilivyoandikwa kwa nukta nundu kwa ajili ya wasioona wakati tukio la utoaji wa tuzo za 'I CAN', pamoja na hafla ya chakula cha mchana katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.

Lazima tuwe na upendo, watu wenye ulemavu wana changamoto nyingi mfano za umasikini ni lazima tuwasaidie kwa vitendo na tujitahidi kuzungumzia uwezo wao pia,” amesema Dkt. Mengi.

Aidha amemuomba aliyekuwa mgeni rasmi, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, vifaa visaidizi kama vile fimbo nyeupe, mafuta ya ngozi, viti mwendo, magongo yanayomlinda mtumiaji asiteleze kwa kuweka mipira maalum na vinginevyo kwa kuwa vimekuwa gharama.

Vitabu vilivyotolewa (I Can I Must I Will) ni toleo la kitabu alichokiandika mwenyewe na kukizindua miezi kadhaa iliyopita, maudhui yake yakiwa ni hamasa kwa jamii kuhusu masuala ya ujasiriamali na uthubutu.