Jumatatu , 2nd Nov , 2020

Dkt Hussein Mwinyi ameapishwa hii leo na Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu katika uwanja wa Amani huko Zanzibar,katika hafla iliyohudhuriwa na marais wastaafu,viongozi wa kitaifa na kimataifa pamoja na wananchi.

Pichani ni Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi (kulia) akila kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu (Kushoto).

Katika hafla hiyo,Dkt. Mwinyi amekula viapo viwili,kikiwemo kiapo cha uaminifu na cha kazi,na kukabidhiwa rasmi kuiongoza Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano,huku akisema anao wajibu wa kuwaongoza Wazanzibar kwa misingi ya haki, uadilifu na usawa

‘’Nitawatumikia Wazanzibar wote bila ya kubagua,kutokana na itikadi za vyama,jinsia,dini au maeneo wanaotoka,na nitafuata misingi ya mila na desturi za wazanzibari’’Amesema Dkt Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar.

Dkt Mwinyi ameongeza kuwa uchaguzi sasa umekwisha kazi iliyoko mbele yetu ni kushirikiana kwa pamoja katika kuiletea maendeleo nchi yetu, kila mmoja ana nafasi na wajibu wa kushiriki katika harakati za maendeleo kwa kuafanya kazi za halali

Aidha, Rais wa awamu ya nane wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi ,alipigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride la heshima,huku Rais anayemaliza muda wake Dkt.Ally Mohamed Shein naye aliagwa kwa kupigiwa mizinga 21.

Rais Dkt. Mwinyi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, alishinda kwa kupata kura 380,402 sawa na asilimia 76.27 ya kura zote zilizopigwa visiwani Zanzibar.