Jumanne , 15th Dec , 2020

Familia ya kijana Masudi Said (24), iliyopo katika Kijiji cha Irungu wilayani Magu mkoani Mwanza, imegoma kuzika mwili wa marehemu kwa takribani siku nane kufuatia kuwepo kwa utata wa kifo cha kijana huyo.

Saidi Haruna ni baba mzazi wa Masudi Saidi.

Familia hiyo inadai kuwa siku ya Desemba 3, 2020, majira ya usiku kijana wao akiwa amelala aligongewa mlango na Mwenyekiti wa Kijiji hicho anayefahamika kama Mashauri Kafura, kwamba aende kwenye ulinzi shirikishi, na kufanikiwa kuondoka nae hadi usiku wa saa nane alipowakabidhi kwa polisi akiwa na wenzake saba.

Akizungumza na EATV, Mama wa marehemu, Pendo William, amesema kuwa mwanaye alichukulia kwa ajili ya ulinzi shirikishi na kupelekwa moja kwa moja kwenye kituo cha polisi Magu, lakini baadaye alipatikana na kesi ya kuvunja koki ya bomba la maji.

"Wamekaa pale kituo cha polisi Magu ndiyo mwanangu akakutwa na kesi ya kuvunja koki ya bomba la maji , kuna askari mmoja wa kike baada ya kufika pale akaanza kumgombeza na kumwitia maaskari wanne wa kiume wakaanza kumsulubu na kumvunja miguu na sikio lake kuchomwa na baadaye tukapata taarifa kwamba amefariki", ameeleza Mama mzazi wa marehemu.

Saidi Haruna ni baba mzazi wa Masudi Saidi, anayedaiwa kufariki akiwa mkononi mwa polisi, amesema wamegoma kuuzika mwili wa mwanae hadi hapo waliosababisha kifo hicho watakapochukuliwa hatua za kisheria.

"Huwezi ukachukua mtu alikuwa mzima halafu ukamzika na majeraha, mimi siwezi kuzika mpaka nielewe huyu aliumia vipi", amesimulia Baba mzazi

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Gideon Msuya, akizungumza na EATV amesema kuwa hana taarifa ya tukio hilo na kuahidi kulifuatilia.