Ijumaa , 16th Nov , 2018

Benki ya Dunia (WB) imeridhia kuipatia Tanzania Dola za Marekani milioni 300 sawa na shilingi bilioni 680.5  kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya sekondari.

Rais Dkt. John Magufuli.

Mradi huo unakusudiwa kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, maabara, nyumba za watumishi na kununua vifaa vya kufundishia. Taarifa iliyotumwa leo Novemba 16, 2018 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema Rais John Magufuli amekutana Ikulu jijini Dar es salaam na Makamu wa Rais wa WB Kanda ya Afrika, Dkt. Hafez Ghanem.

Katika mazungumzo yao, Rais Magufuli amesema pamoja na kuridhia kutoa fedha za mradi huo, Benki hiyo inaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.

Makamu wa Rais wa WB Kanda ya Afrika, Dkt. Hafez Ghanem, akiwa na Rais Dkt. Magufuli, Ikulu jijini Dar es salaam.

Amesema miradi hiyo yenye thamani ya Dola za Marekani 5.2 bilioni sawa na zaidi ya Sh13 trilioni inatekelezwa kutokana na uhusiano na ushirikiano mzuri baina yake na Tanzania. Dkt. Ghanem amesema katika mazungumzo hayo wamejadili juu ya maendeleo ya miradi hiyo na kazi nzuri ambayo inafanywa na Tanzania kuimarisha uchumi.

Namshukuru Dk Hafez Ghanem na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania, baadhi ya watu wasiotutakia mema walisema zimefyekelewa mbali, kwa hiyo amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha” amesema Rais Magufuli.