Halima Mdee alianzisha tena

Jumanne , 13th Feb , 2018

Mbunge wa jimbo la Kawe (CHADEMA) Mhe. Halima Mdee amefunguka na kudai katika uchaguzi huu wa marudio unaotarajiwa kufanyika Jumamosi (Februari 17) anataka haki itendeke kwa wagombea ili amani na utulivu wa nchi uendelee kuwepo.

Mdee ametoa kauli hiyo akiwa anamuombea ridhaa mgombea wao wa jimbo la Kinondoni Salum Mwalimu ili aweze kuwa muwakilishi wa wananchi hao na kusema safarii hawatakubali kuona dhuluma ikiendelea kutendeka za kuiba kura za mgombea fulani na kwenda kwengine kama walivyozoelea kuwafanyia.

"Huu uchaguzi tunataka watawala wajue kwamba kila mbinu wanayoifanya tunaijua lakini hakuna marefu yasiyokuwa na ncha. Tunataka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Taifa (NEC), Polisi pamoja na wasimamizi wa uchaguzi ambao watakaotumwa na CCM wajue iwe jua, mvua, matope au mchanga, tunahitaji mwenye haki yake apewe", amesema Mdee.

Pamoja na hayo, Mdee ameendelea kwa kusema "Maulid Mtulia akishinda apewe Mtulia, Salum Mwalimu akishinda apewe Salum Mwalimu. Wananchi tumechoka kufikilia kuja hapa, wananchi tumechoka kufanywa mazuzu wakati tunajielewa.Tunataka mfumo wa demokrasia uwaachiliwe ili amani na utulivu wa nchi yetu ipate kubaki kwa sababu ikivunjwa haitabaki na hakuna mtu atakayepona".

Kwa upande mwingine, Halima Mdee amesema katika nchi zilizoendelea kidemokrasia huwa hakuna vyama vinavyotawala milele wala kuwadanganya wananchi.