Alhamisi , 23rd Jan , 2020

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema kuwa ataendelea kumuunga mkono Rais Magufuli hata baada ya yeye kumtengua na kwamba hatua aliyoichukua Rais Magufuli ni njema kwani ina lengo la kujenga safu ya Serikali ya awamu ya Tano.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola

Lugola ameyabainisha hayo muda mfupi tu tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, kutangaza hadharani kuwa amepokea barua ya kujiuzulu kwake.

"Mheshimiwa Rais ndiye aliyeniteua  kwenye Baraza la Mawaziri na ndiye ameona anipumzishe, kwangu mimi ni jambo la faraja, hatua alizozichukua ni nzuri zina lengo la kujenga vizuri safu ya Serikali, kama Mbunge niliyepata nafasi ya kumsaidia Rais, nitaendelea kumsaidia na kutumikia Serikali ya awamu ya Tano kwa heshima kubwa" amesema Waziri Lugola.

Katika hotuba yake leo Januari 23, 2020, Rais Magufuli, wakati akizindua nyumba za Maaskari Magereza zilizopo Ukonga Jijini Dar es Salaam, alionesha kutofurahishwa na mwenendo wa viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, baada ya kusaini mradi Nje ya Nchi, wenye thamani ya zaidi ya Trilioni 1, ambao haukupitishwa na Bunge.