Jumapili , 20th Aug , 2017

Mbunge wa jimbo la Kigoma Ujiji Mh. Zitto Kabwe amekingia kifua kauli inayotolewa na serikali ikiwashutumu vyama vya upinzani kushiriki na kutoa taarifa za ndege kuzuiliwa nchini Uingereza, na kusema kuwa kama wananchi wana kila haki ya kuhoji.

Mh. Zitto Kabwe

Akijibizana na baadhi ya wananchi kwenye ukurasa wake wa twitter, Zitto Kabwe ameandika akisema suala kama hilo ni lazima watu wahoji, na sio kama hawapendi maendeleo yanayofanywa na uongozi wa Rais Magufuli, isipokuwa wanataka serikali ifanye vitu kwa uhakika zaidi, ili kuepusha kujiingiza kwenye hasara na migogoro kama hiyo.

“Watu ni lazima wahoji mtake mistake, hakuna anayetaka msubiri, tunataka mfanye Kwa  uhakika, tutaendelea kuhoji na lazima  serikali ijibu”, aliandika Zitto Kabwe.

Mh. Zitto Kabwe aliendelea kuandika “hatukutaka mnunue ndege hovyo hovyo, lakini ndege tunataka na tunapanda, mkihojiwa mnaleta viroja, jibuni hoja tu viroja vya nini ?”, aliandika Zitto Kabwe.

Baada ya muda mfupi Mh. Zitto Kabwe alihamia kwenye ukurasa wake wa facebook na kuandika.." Suala la ndege yetu kuzuiwa Canada lisifanywe ni suala la ushabiki kama ushabiki wa mpira. Ni suala la nchi hili na mjadala wake uwe na hadhi hiyo.
Kitendo cha Msemaji wa Serikali kulaumu wanasiasa kwa jambo la kisheria kama hili ni utoto, hakuna mwanasiasa anayeweza kushirikiana na kampuni za kigeni kuhujumu nchi".

Siku ya tar 18 Agosti Mbunge wa Singida Mashariki na mwanasheria mkuu wa CHADEMA Mh. Tundu Anthipas Lissu, alitoa taarifa kuwa kuna mali za Tanzania zimezuiliwa nchini Canada kutokana na deni ambalo serikali inadaiwa na kampuni ya ukandarasi.

Baada ya taarifa hizo kutolewa na mbunge huyo, serikali ikathibitisha uwepo wa suala hilo na kuongeza kuwa kuna ya watu  wa vyama vya upinzani wameshirikiana na makampuni ya nje kufungua kesi kama hizo, ili kuweka vikwazo kwa serikali kuweza kufanikisha mipango ya maendeleo inayofanywa na serikali ya awamu ya tano.