Jumapili , 21st Dec , 2025

“Mtuhumiwa na wenzake ambao wanaendelea kutafutwa walipanga kufanya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Tunduma na viunga vyake”

Jeshi la Polisi mkoa wa Songwe limetoa ufafanuzi kuhusu taarifa zisizo sahihi zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Henry Mboya, zikidai kuwa hajulikani alipo baada ya kukamatwa na Polisi.

Taarifa iliyotolewa leo Disemba 21 na Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe imesema kuwa Henry Mboya, Mkazi wa Tunduma, wilaya ya Momba mkoa wa Songwe alikamatwa na anaendelea kushikiliwa na Polisi kwa tuhuma za jinai zinazomkabili.

“Mtuhumiwa na wenzake ambao wanaendelea kutafutwa walipanga kufanya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Tunduma na viunga vyake”, taarifa ya polisi imefafanua na kuongeza kuwa, katika upekuzi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwenye makazi yake, amekutwa na Bastola bandia na koti moja lenye nembo ya SUMA JKT, vitu ambavyo alikuwa akivitumia kwa uhalifu.

Kufuatia taarifa zisizo sahihi kusambazwa mitandaoni, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa hizo ambazo hazitoki kwenye mamlaka au vyanzo rasmi.