Jumanne , 17th Jul , 2018

Rais Dkt. John Magufuli amefunguka na kudai nchi za Afrika zimeisaidia China kupata kiti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jambo ambalo limefanya taifa hilo kuwa na ushirikiano mzuri na kutoa mikopo isiyokuwa na masharti magumu.

Rais Dkt. John Magufuli

Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo leo Julai 17, 2018 wakati alipofungua mkutano maalum wa majadiliano kati ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na vyama vya siasa vya nchi mbalimbali za Afrika unaofanyika kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam na kusema anaishukuru CPC na vyama vyote vya Afrika kwa kuichagua Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mwenyeji wa mkutano huo ambao utatoa fursa ya majadiliano ya namna vyama vya siasa vitakavyosaidia serikali zao.

"Ni jambo la kufurahisha ni kwamba uhusiano wetu umejengwa kwenye misingi ya kuelewana na kuheshimiana, na ndio sababu misaada ya China kwetu imekuwa haiambatani na masharti magumu, hili ndilo hasa sote tunalitaka, ushirikiano ambao sote tunajiona tupo sawa na sote tunanufaika", amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ushirikiano huu wa China na Afrika, bado kuna changamoto kubwa ya kukuza zaidi uhusiano katika masuala ya kiuchumi kwa kuhakikisha Afrika inauza bidhaa nyingi zaidi nchini China, China inaongeza uwekezaji barani Afrika hususani katika kilimo, viwanda na madini, na pia kukuza ushirikiano katika ujenzi wa miundombinu ya usafiri na umeme.

Kwa upande wa Mhe. Song Tao ameishukuru CCM kwa kuandaa mkutano huu mkubwa ambao utasaidia kujadiliana na kubadilishana uzoefu kati ya CPC na vyama vya siasa vya Afrika juu ya namna bora ya kuimarisha sera zake ili ziweze kuleta mabadiliko ya kiuchumi kama ambavyo CPC ilifanya.

Mtazame hapa chini Rais Magufuli akiongea mengine zaidi pamoja na fursa zilizotolewa na nchi hiyo kwa Tanzania.