Alhamisi , 2nd Feb , 2023

Kitengo cha kuhudumia waathirika wa dawa za kulevya kilichopo hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mwananyamala kimesema kinahudumia waathirika wa dawa za kulevya  1,459 kwa siku kwa kunywa methadone huku idadi kubwa ya waathirika wa dawa hizo wakitokea Kinondoni.

Akizungumza na EATV leo Februari 2, 2023, daktari wa kitengo hicho kutoka katika hospitali hiyo Dkt Rashida Hashim, amesema hali ni mbaya kwa sababu idadi kubwa ya vijana wameathirika na dawa za kulevya na tangu walipoanza kliniki hiyo wamekuwa na waathirika wa dawa hizo za kulevya 3,411 huku wanaume wakiwa ni 1,360 na wanawake ni 99 ingawa kila siku wanapokea waathirika wapya wa dawa za kulevya watatu mpaka wanne. 

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii katika kitengo hicho Hafsa Rashid Mtwange, amesema licha ya kuwahudumia waathirika wa dawa za kulevya lakini ipo changamoto kwa baadhi yao kuacha kutumia methadone kwa sababu mbalimbali ikiwemo mazingira anayoishi kwani anajaribu kuacha kutumia dawa za kulevya  lakini anaporudi mtaani anakutana na vijana wenzake wanaitumia dawa hizo na kujikuta nae anarudia kutumia.

Nao waathirika wa dawa za kulevya wakizungumza wamesema tangu walipoacha kutumia dawa hizo afya zao zimekuwa zikiendelea vizuri tofauti na walivyokuwa wakitumia dawa za kulevya.