Jumatano , 29th Nov , 2017

Mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP) Simon Sirro amewataka wazazi na walimu wilayani Kibiti na Rufiji, kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola juu ya kutoweka kwa wanafunzi zaidi ya 1,300 wakati wa matukio ya kiuhalifu yaliyotokea katika wilaya hizo.

Katika ziara yake ya kikazi wilayani Kibaha, mkoani Pwani IGP amezungumza na wazazi, walimu pamoja na viongozi wa mashirika ya umma,wazee maarufu, wastaafu mbalimbali na kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo.

IGP Sirro amewataka wazazi husika na walimu wa shule za msingi na sekondari ambazo wanafunzi walikuwa ni watoro ama hawajaripoti shule kwa miezi kadhaa kutoa taarifa kwani wapo baadhi ya watoto wanaotumika kufundishwa uhalifu hata wakutumia silaha na watu wasiowema.

Kamanda Sirro ameeleza kuwa taarifa ya wanafunzi zaidi ya 1,300 mkoani hapo kuwa ni watoro na hawajulikani walipo hivyo wazazi washirikiane kusaidia jeshi la polisi kujua walipo.

“Kuna baadhi misikiti,makanisa yanadaiwa yanayotumia watoto hawa katika masuala ya kiuhalifu hivyo kuna kila sababu ya kuingia ndani kutafuta suluhu”, amesema Sirro.

Mkuu huyo wa jeshi la polisi amewahakikishia wananchi mkoani Pwani kuwa silaha zote zilizochukuliwa na wahalifu wa ovyo ovyo huko Kibiti na Mkuranga zimerudi zote mkononi mwa dola na kusambaratisha mtandao wa kiuhalifu na wanaendelea kushirikiana na Msumbiji kutokomeza uhalifu.