Jumapili , 4th Mei , 2014

Jaji mstaafu wa mahakama kuu ya Tanzania, Mark Bomani, amewataka wana habari nchini kufanya kazi bila woga pamoja na kukataa kununuliwa, hii ikiwa ni pamoja na kuendelea kupigania sheria ya uhuru wa vyombo vya habari.

Jaji mstaafu wa mahakama kuu ya Tanzania, Mark Bomani

Akizungumza katika siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo kitaifa imefanyika jijini Arusha, jaji Bomani amewapongeza wadau wa tasnia ya habari kwa jinsi wanavyotekeleza majukumu yao ya kuelimisha, kuhabarisha, kuburudisha na kukosoa jamii.

Amefafanua kuwa tasnia ya habari ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo na ustawi wa taifa, ambapo amesema kwa Tanzania, tasnia ya habari ni muhimu sana kipindi hiki cha mchakato wa katiba kwani mchango wa vyombo vya habari unahitajika kuelimisha sio tu wananchi wa kawaida, bali hata viongozi na wabunge.