Alhamisi , 31st Mar , 2022

Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma imewahukumu jela miaka miwili, watu wawili Tumaini Thomas na Jonas Mbilimi, wakazi wa Nyachenda wilayani Kasulu baada ya kumuua mwenzao aliyemimina pombe yao ya kienyeji aina ya Wanzuki wakiwa wanalewa kwenye kilabu cha Pombe.

Picha ya mfano wa mtu anayemimina pombe ya kienyeji

Kesi ya mauaji ya bila kukusudia namba 14 ya mwaka 2021 Jamuhuri dhidi yao ikisikilizwa na jaji mfawidhi wa mahakama hiyo Lameck Mlacha, mnamo Septemba 5, 2020 washtakiwa wakiwa wanakunywa pombe  marehemu akanyanyuka na kumimina pombe hiyo hali iliyosababisha ugomvi na  marehemu alikimbia wakamuangusha na kumkanyaga na miguu pamoja na kumpiga na kigoda kichwani.

Upande wa Jamuhuri uliwasilisha ushahidi mashuhuda wa tukio hilo, Askari na ndugu pamoja na ushahidi wa daktari ulio eleza  fuvu la kichwa upande wa kushoto lilivunjika na kifo kilisababishwa na kuvuja damu nyingi kwenye ubongo.

Upande wa utetezi ukiwakilishwa na wakili Joseph Mathias washtakiwa walisema walikuwepo wakati wa tukio na ugomvi ulivyoibuka mmoja wao aliamua ili wasigombane kisha wakaenda nyumbani na baadae kupata taarifa ya kifo hicho.

Jaji Mlacha baada ya kuangalia ushahidi wa pande zote amesema washtakiwa wameidanganya mahakama kwa kuwa mashahidi walio kuwepo walishuhudia tukio pamoja na maelezo ya marehemu kwa familia kabla hajafa hivyo ikawakuta na hatia ya mauaji ya bila kukusudia na wakili wa Jamuhuri Benedict Kivuma  akaomba adhabu kali.

Upande wa utetezi ukaiomba mahakama kutumia mwezi wa Kwarezima kuwapunguzia adhabu kwani wana umri mdogo miaka 28-29, wanategemewa na familia na watoto wao, hawana rekodi ya kutenda makosa mengine na mazingira ya kosa wote walikuwa wamelewa.

Jaji Mlacha akasema ulevi sio utetezi wa jinai yoyote lakini kutokana na mazingira ya kosa lilivyo tendeka  akawahukumu kwenda jela miaka miwili.