Jumamosi , 30th Jan , 2016

Rais Magufuli amempongeza Nahodha wa timu ya Taifa ya Soka Tanzania (Taifa Stars) Mbwana Samatta, kwa kusajiliwa na timu ya KRC Genk inayocheza ligi kuu ya Ubelgiji, Barani Ulaya.

Mwana Samatta baada ya kutambulishwa Genk

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Nahodha wa timu ya Taifa ya Soka Tanzania (Taifa Stars) Mbwana Samatta, kwa kusajiliwa na timu ya KRC Genk inayocheza ligi kuu ya Ubelgiji, Barani Ulaya.

Katika Salamu hizo kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Rais Magufuli amesema Mbwana Samatta ameijengea heshima Tanzania na kuitangaza kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Magufuli amesema mafanikio ya Samatta kwenda kucheza katika ligi kubwa duniani, kunafungua milango ya wanasoka wengine wa Tanzania kujiunga na timu kubwa duniani, ambako licha ya kujipatia ajira zenye kipato kizuri, kunaiwezesha kuinua soka lake.

Taarifa hiyo imemnukuu Rais Magufuli akisisitiza "Nimefurahishwa na mafanikio anayoendelea kuyapata Mbwana Samatta, nawaomba wanasoka wote Tanzania wayachukue mafanikio haya kama changamoto ya kufanya vizuri na kuzivutia timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi"

Aidha, Rais Magufuli amemtaka Mbwana Samatta kuongeza juhudi akiwa katika timu yake hiyo mpya ya KRC Genk, na amemuombea mafaniko mema yeye mwenyewe na timu yake.

Kabla ya kujiunga na timu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta alikuwa mchezaji wa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako alifanya vizuri na kufanikiwa kuwa Mfungaji bora wa ligi ya mabingwa Barani Afrika na pia kutwaa tuzo ya Mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani.