Jumatano , 11th Jul , 2018

Jeshi la Polisi limefanikiwa kumkamata mwalimu wa shule ya sekondari Loliondo, Erick Kalaliche mkoani Lindi ambaye anatuhumiwa kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wake wa kidatu cha tatu katika shule ya sekondari Loliondo kabla ya mwalimu huyo kuhamishwa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng'anzi

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng'anzi leo Julai 11, 2018 wakati akizungumza na www.eatv.tv baada ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha kutoa agizo la kutafutwa na kukamatwa kwa mwalimu huyo ambaye ametenda kosa la jinai na kuhamia katika shule nyingine.

"Agizo la Naibu Waziri wa Elimu tumelipokea na kama inavyofahamika kuwa kumpa ujauzito mwanafunzi ni kosa la jinai na jarada limeshafunguliwa la kupeleleza tukio hilo kwasababu baada ya kuwasiliana na Mkurugenzi wake yule
mwalimu alipewa uhamisho tangu mwaka 2017 lakini tumewasiliana na wenzetu katika kituo chake kipya kule Lindi na wametuambia kwamba wamefanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo leo hivyo tunafanya mpango wa kurudishwa huku kwenye kesi yake"
, amesema Kamanda Ng'anzi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu William Ole-Nasha amesisitiza kuwa, Wizara yake haiwezi kuvumilia walimu wanaofundisha watoto ambao pia ni kama wazazi wanaofumbia macho vitendo vichafu ambavyo vinarudisha nyuma sekta ya elimu na juhudi za serikali za kuhakikisha watoto wa kike haki yao ya elimu.