Ijumaa , 15th Jul , 2016

Serikali mkoani Mbeya imelipongeza jeshi la polisi mkoani Mbeya kwa kuweza kudhibiti tukio la ujambazi lililokuwa lifanyike Julai 11 mwaka huu wilayani Rungwe na pia kuua majambazi wawili na kukamata bunduki zao.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla

Mnamo Julai 11 majira ya mchana jeshi la polisi wilayani Rungwe lilifanikiwa kuwaua majambazi wawili na kuwajeruhi wengine ikiwa ni baada ya jeshi hilo kupata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya uwepo wa watu waliokuwa wamepanga kuvamia Matawi ya benki za NMB na NBC katika mji wa Tukuyu.

Kutokana na kuimarishwa kwa ulinzi kwenye matawi ya benki hizo jambazi hao waliamua kubadili mwelekeo na kunuia kwenda kuvamia nyumba ya mfanyabiashara mmoja katika kijiji cha Makandana kilichopo nje kidogo ya mji wa Tukuyu na ndipo wakajikuta wameingia kwenye mtego wa polisi ambao bila hiana waliwashambulia na kuwaua wawili kati yao.

Kufuatia tukio hilo,Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla, amelipongeza jeshi la polisi akisema linaonekana kujipanga ipasavyo kukabiliana na matukio ya ujambazi sanjari na agizo alilolitoa siku alipotembelea jeshi hilo na kuagiza kutokuwepo kwa urafiki baina ya Askari na Majambazi akisema anayekuja na moto muwashie moto.

Makalla alitoa pongezi hizo alipozungumza na wakazi wa kata ya Mpuguso wilayani Rungwe alipokwenda kuzindua ujenzi wa kituo cha afya cha kata hiyo na kubainisha kuwa jitihada hizo za polisi lazima ziungwe mkono na jamii yote.
Amewapongeza raia wema wanaoendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ikiwemo kutoa taarifa kama walivyofanya kwa tukio la Rungwe akisema hiyo ndiyo nyenzo muhimu itakayowezesha mafanikio katika kupambana na uhalifu.

Amewataka wakazi wa Rungwe na maeneo ya jirani,kufuatilia wagonjwa walio na majeraha waliopo majumba,hospitalini na kwa waganga wa tiba za asili akisema upo uwezekano mkubwa wa majambazi wawili waliojeruhiwa kwa risasi wakati wa mashambuliano na polisi wanaendelea na matibabu.

Kwa wale wanaomiliki silaha pasipo kuzihakiki pamoja na wanaotengeneza kinyemela bunduki,amewataka kuachana na kazi hizo kwakuwa si muda mrefu vyombo vya dola vitaendesha oparesheni ya kukagua.

Sauti ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla