Alhamisi , 21st Mei , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, ameagiza kuwa mtu yeyote atakayepokea vifaa vya kupambana na Virusi vya Corona, vikishapimwa na Maabara Kuu ya Tanzania na kukutwa vina Virusi vya hivyo, basi ashitakiwe na apewe kesi ya jinai.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli ameyabainisha hayo leo Mei 21, 2020, Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma, mara baada ya kuwaapisha Mabalozi wa nchi mbalimbali , Mkurugenzi wa TAKUKURU na Katibu Tawala Mkoa na kuongeza kuwa vitu vya bure vina gharama.

"Kwa mtu yeyote atakayepewa vifaa vya kuzuia Corona, halafu mkavipima mkakuta vina Corona, huyo mtu apelekwe kwenye kesi ya jinai, hata mauaji, Watendaji wajiepushe kupokea pokea, tutatengeneza Barakoa zetu na tutatumia vifaa ambavyo vitakuwa tested na Maabara zetu, Corona inaisha lakini tusije tukapandikiziwa" amesema Rais Magufuli.

Awali wakati wa hotuba yake, Rais Magufuli amekiri kumpa usumbufu mkubwa sana Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, na kumpongeza kwa namna ambavyo alikuwa mstari wa mbele katika mapambano hayo licha ya kwamba hana taaluma ya Udaktari.