Juhudi ziongezwe kumkomboa mwanamke- Maria Sarungi

Jumatano , 9th Mar , 2016

Mkurugenzi wa kampuni ya Compass Communications ambaye pia ni mdau wa masuala ya kijamii nchini Bi. Maria Sarungi Tsehai amesema jitihada zinahitajika zaidi hasa uwekezaji kwa elimu kwa watoto wa kike ili kuweza kufikia 50 kwa 50 mwaka 2030.

Bi Sarungi ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na EATV kuhusu siku ya wanawake duniani siku ambayo kauli mbiu kwa mwaka huu inasema 50 KWA 50 mwaka 2030 Tuongeze Jitihada.

''Ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa ni lazima wadau wote kuunganisha nguvu na kuhakikisha wanawake wanapata elimu na habari kuhusiana na mambo mbalimbali yanayowahusu, kwa kuzingatia maeneo yote ya mijini na vijijini''

Kwa upande wa mila potofu kuhusu umiliki wa ardhi na usawa katika maeneo ya kazi Bi Sarungi amesema kuna haja ya serikali na wadau kuangalia upya suala la mishahara kwa upande wa wanawake kwani pamoja na shughuli nyingi anazofanya mwanamke katika jamii mshahara wake katika kitengo kimoja na mwanaume si sawa jambo ambalo linawarudisha nyuma wanawake.

Aidha amepongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuwa na makamu wa Rais mwanamke Mh Samia Suluhu ambaye Rais John Pombe Magufuli amemuamini na kumtuma katika mikutano muhimu katika maeneo mbalimbali na kuonyesh uwezo mkubwa katika uwakilishi huo.

Hivyo amesisitiza kuwa wanawake wote ambao wamepata nafasi za uongozi katika serikali kuhakikisha wanafanya kazi kwa uwezo wa hali ya juu ili iwe chachu ya jamii kuthamini michango yao katika nafasi walizopewa.