Jumapili , 8th Nov , 2020

Baada ya jana Novemba 7, 2020, mgombea urais wa Chama Cha Democratic, Joe Biden, kutangazwa mshindi wa kiti cha urais wa Taifa la Marekani, akimshinda Rais aliyekuwa madarakani Donald Trump, Biden amesema kazi itakuwa ngumu lakini ataifanya kwa nguvu zote.

Joe Biden akiwa na Makamu wa Rais Kamala Harris

Biden ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter kwa kuandika, ''Marekani nashukuru kwa kunichagua kuongoza taifa letu zuri, natambua kazi itakuwa ngumu ila naahidi nitakuwa Rais wa wote, walionipigia kura na ambao hawajanipigia''.

Joe Biden ambaye anakuwa Rais wa 46 wa Marekani, aliongeza kuwa, ''nitaulinda huu uaminifu mkubwa mliopatia''.

Aidha katika mahojiano na vyombo mbalimbali Rais huyo mteule wa Marekani alieleza furaha ya ushindi wake wa kihistoria katika uchaguzi wa Rais.

'Tumeshinda kwa kura nyingi kuwahi kupigwa kwa mgombea wa Urais kwenye historia ya taifa hili, kura milioni 74. Ninaahidi kuwa Rais wa Marekani na sio wa majimbo ya Bluu au Nyekundu na Marekeani itakuwa na heshima tena''.