Jumatatu , 10th Aug , 2020

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng'wilabuzu Ludigija amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, kwa kuendelea kumuamini na kumpa nafasi mbalimbali za uongozi huku akiwaomba watendaji wenzake wapya kumpa ushirikiano ili aweze kutimiza kazi aliyopewa kwa ufanisi.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Agosti 10, 2020, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio, ikiwa ni siku moja tu imepita tangu Rais Magufuli amteue kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, kutoka katika nafasi ya Ukurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni.

"Nimshukuru sana Mh Rais kwa kuendelea kuniamini, tumekuwa hapo Manispaa ya Kigamboni tumefanya mambo makubwa lakini kwa jukumu hili jipya ni jukumu kubwa na Ilala ni wilaya ya kibiashara na wananchi wengi wanategemea sana Ilala niwaombe watumishi wa Ilala kunipatia ushirikiano ili tuhakikishe kwamba tunawatumikia wananchi wetu" amesema Ludigija.

Aidha Ng'wilabuzu akataja vipaumbele vyake, "Niseme kwamba mimi ni mtu ambaye napenda sana kutembea Site nijue eneo ambalo nalisimamia lakini pia nitahakikisha napata muda wa kuwa ofisini ili niweze kuwahudumia makundi yote wale wenye shida ya mtu mmoja mmoja nao watapata kuhudumiwa".