Hatua ya awali ya usikilizaji wa kesi 17 za kupinga matokeo ya uchaguzi wa Uwakilishi, zilizofunguliwa na waliokuwa wagombea wa Chama cha ACT WAZALENDO katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imekamilika katika Mahakama Kuu ya Zanzibar iliyopo Tunguu.
Mrajisi wa Mahakama Kuu, Valentine Katema, amesema baada ya taratibu zote za awali kukamilika, ofisi yake itayawasilisha majalada ya kesi hizo kwa Jaji Mkuu wa Zanzibar kwa ajili ya kupangiwa majaji watakaosikiliza mashauri hayo.
Mrajisi Katema ameahirisha kikao cha leo, akieleza kuwa jukumu lake ni kukamilisha hatua za awali kabla ya Jaji Mkuu kuendeleza mchakato wa kisheria unaofuata.
Kesi hizo 17 zinahusu pingamizi dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa Uwakilishi, ambapo wagombea wa ACT WAZALENDO wanapinga kutangazwa kwa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa washindi. Kati ya kesi hizo, tisa zimefunguliwa Unguja na nane Kisiwani Pemba.
Wagombea wote 17 walihudhuria mahakamani wakisindikizwa na viongozi wa kitaifa wa chama pamoja na wanachama wao. Baada ya utambulisho wa mawakili wa pande zote mbili, Wakili wa waombaji, Suleiman Abdalla, aliomba mahakama iwawezeshe walalamikiwa kuwasilisha hati za majibu ya majibu, kama ilivyoahidiwa katika kikao cha awali kilichofanyika tarehe 10 Disemba 2025.
Upande wa walalamikiwa uliomba muda wa kupitia majibu hayo ili kubaini iwapo kuna haja ya kuwasilisha majibu ya ziada.
Walalamikiwa katika kesi hizo ni Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Upande wa serikali uliwakilishwa na jopo la wanasheria likiongozwa na Wanasheria Waandamizi Salim Said, Mbarouk Suleiman Othman, Ali Issa Abdalla na Maulid Ame Mohamed kwa niaba ya ZEC.
Kwa upande wa Pemba, kesi hizo zinatarajiwa kutajwa tena tarehe 23 Disemba 2025 kwa ajili ya kukamilisha taratibu za awali.
Majimbo yanayopinga matokeo Unguja ni pamoja na Nungwi, Kijini, Mkwajuni, Chaani, Tumbatu, Bumbwini, Mtoni, Mwera, Welezo, Mwanakwerekwe, Pangawe, Kiembesamaki, Amani, Chumbuni, Mpendae, Malindi na Makunduchi.
Kwa Pemba ni majimbo ya Kojani, Micheweni, Wawi, Chake Chake, Chonga, Kiwani, Chambani na Mkoani.
