Shauri la kesi ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo, linalosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu limeahirishwa tena hadi Disemba 30 baada ya Upande wa Jamhuri kushindwa kuwasomea washitakiwa maelezo ya mashahidi na vielelezo baada ya kubainika kuwa baadhi ya nyaraka hazipo katika mfumo wa mahakama.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, Wakili wa Serikali, Glory Kilawe amebainisha leo Disemba 19, 2025 kuwa shauri hilo lililetwa mahakamani kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya mashahidi pamoja na vielelezo, hata hivyo baada ya kupitia jalada halisi la kesi na taarifa zilizopakiwa katika mfumo wa mahakama, ilibainika kuwa baadhi ya nyaraka muhimu hazipo.
Kutokana na hali hiyo, ameomba mahakama ipange tarehe nyingine ili upande wa Jamhuri ufanye marekebisho ya nyaraka hizo ombio ambalo limekubaliwa na Mahakama na kuliahirisha shauri hilo hadi Desemba 30, mwaka huu.
Katika kesi hiyo, wafanyabiashara sita wanakabiliwa na shtaka la mauaji bila kukusudia, yaliyotokana na kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo, Dar es Salaamakiwemo Lendela Mdete, mkazi wa Mbezi; Zenabu Islam maarufu kama Zaibanu, mkazi wa Kariakoo; Ashour Ashour, mkazi wa Ilala; Soster Nziku, mkazi wa Mbezi Beach; Aloyce Sangawe, mkazi wa Sinza; pamoja na Stephen Nziku, mkazi wa Mbezi Beach.
Washitakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 16, 2024, katika Mtaa wa Mchikichi na Kongo, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, ambapo wanadaiwa kushindwa kutimiza majukumu yao, hali iliyosababisha kuporomoka kwa jengo hilo.
Kutokana na tukio hilo, watu 31 walipoteza maisha, akiwemo Said Juma, Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu na Chatherine Mbilinyi.
Wakati kesi hiyo ikitarajiwa kuendelea kusikilizwa, meelezwa mahakamani hapo kuwa upande wa Jamhuri unatarajia kuwasilisha mashahidi 55 na vielelezo 54.
