Jumatatu , 19th Oct , 2015

Zikiwa zimebaki siku 5 tu kufikia Oktoba 25 ambapo Uchaguzi Mkuu utafanyika kampeni za kugombea nafasi mbalimbali zimeendelea kushika kasi huku wagombea urais wakiendelea kutoa ahadi zaidi wakisisitiza kilimo na Viwanda.

Mgombea Urais kupitia chama cha CHAUMMA, Hashim Rungwe

Akiwa mkoa wa Mtwara mgombea urais kupitia chama cha CHAUMMA, Hashim Rungwe amesema kuwa endapo wananchi watampa ridhaa ya kuiongoza nchi basi katika sekta ya kilimo ataanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa helkopta na ndege.

Awali, mgombea mwenza wa chama hicho, Issa Abasi Hussein, aliwataka wananchi hasa akina mama kuto shawishika na pesa kidogo kutoka kwa baadhi ya makada wa CCM ili kuwapa madaraka ya kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano huku wao wakitaabika na hali ngumu ya maisha.

Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara jijini Mbeya kwenye viwanja vya shule msingi Ruanda Nzovwe Mgombea Urais wa UKAWA kupitia CHADEMA, Edward Lowassa amesema kuwa akipata ridhaa ya watanzani Oktoba 25 mwaka huu Lowassa anaahidi kuunda serikali itakayofanya kazi kwa kasi ya "speed 120" kwa saa.

Lowassa amesisitiza kuwa endapo ataingia madarakani atahakikisha mpango wake wa kupandisha hadhi hospitali za wilaya kuwa za rufaa kwa kuboresha vitendea kazi na vifaa tiba.

Waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye akautaka umma wa watanzania kumpigia kura mgombea wa UKAWA na kwamba ataibadilisha Tanzania kutoka kwenye umasikini.

Kwa upande wake Mgombea wa Chama cha Mapinduzi CCM, Dkt. John Pombe Magufuli akiwa jijini Mwanza wilayani Misungwi aliwaahidi wakazi wa jiji hilo kufufua viwanda vya pamba ili kukuza uchumi wa wakulima hao na nchi kwa Ujumla.

Aidha Dkt. Magufuli ameongeza kuwa katika serikali yake atahakikisha mawaziri atakaowachagua akiwemo waziri Mkuu lazima wawe wazalendo na kuwatumikia wananchi huku akiwaponda viongozi walitoka chama hicho na kuasisi na kuwaambia wananchi kuwa ccm haijafanya chochote.