Jumatano , 15th Jul , 2020

Mbunge wa Ubungo kupitia CHADEMA aliyemaliza muda wake Saed Kubenea, amesema kuwa miongoni mwa sababu zilizopelekea yeye kutokuchukua fomu ya kuwania Ubunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya chama hicho ni pamoja na migawanyiko iliyopo ndani ya chama sanjari na yeye kusakamwa.

Saed Kubenea

Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 15, 2020, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital na kueleza kuwa licha ya kwamba hakuchukua fomu ya kuwania Ubunge kupitia CHADEMA, lakini hiyo haimzuii yeye, kugombea jimbo hilo kupitia chama kingine kwa kuwa michakato ndani ya vyama vingine haijafungwa.

"Ni kweli sikuchukua fomu ya kuwania Ubunge wa Jimbo la Ubunge kupitia CHADEMA na kwamba mimi si miongoni mwa wagombea wa CHADEMA watakaopigiwa kura leo kwenye mkutano mkuu wa kura za maoni kwa ajili ya kumpata mgombea wa Ubungo, lakini hiyo hainizuii mimi kugombea kupitia chama kingine, na sababu ni nyingi ikiwemo migawanyiko ndani ya chama na kusakamwa" amesema Kubenea.