Jumamosi , 14th Sep , 2019

Waziri kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, amesema Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Kangi Lugola anayokazi kubwa ya kufanya ili kuweza kumdhibiti mwanaharakati Cyprian Musiba kwa kuwa inaonesha mtu huyo ana nguvu kubwa.

Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital, leo Septemba 14, 2019, Lema ameeleza kuwa onyo pekee lililotolewa jana na Kangi dhidi ya mwanaharakati huyo halitoshi na ilipaswa kuwepo watu wanaowajibishwa kwa kuwa waliruhusu Musiba aendelee kutoa maneno ya kashfa kwa viongozi mbalimbali.

''Musiba atakuwa nani, Musiba atakuwa ni Papa, Musiba atakuwa ni Yesu, Kangi anatakiwa ajue huyu Papa anayemuendesha huyo Yesu ni nani, akijua hilo atajua 'kudeal' na hilo jambo vizuri'' amesema Lema.

Mbunge Lema ametoa kauli hiyo ikiwa ni masaa machache tu tangu Waziri Lugola, alipotoa onyo kwa Mwanaharakati huru Cyprian Musiba, kwamba aache kuwaaminisha watanzania kwamba Serikali inamtuma kufanya uanaharakati wake na endapo ataendelea jeshi la polisi halitosta kumchukulia hatua kali.