Lema amtaka Polepole agombee naye Arusha 2020

Jumanne , 19th Nov , 2019

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amesema hana mpango wowote wa kugombea jimbo lolote mkoani Kilimanjaro, bali atagombea tena jimbo la Arusha Mjini, na kudai atashinda kwa kishindo.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Mbunge Lema ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na EATV na EA Radio Digital, kuhusiana na kauli iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, kuwa Mbunge huyo huenda akahamia jimbo jingine kwenye Uchaguzi wa 2020.

Lema amesema kuwa "Kwanza Polepole inabidi afahamu Ubunge kwangu si ajira, naweza kufanya kazi hata nikiwa mtumishi wa Mungu, au Mwalimu wa Sunday School, ila niweke wazi siwezi kwenda kugombea Kilimanjaro, nitagombea palepale Arusha Mjini."

"Tena niwaambie tu nitagombea palepale Arusha Mjini, na niwaambie CCM wamuweke mgombea yeyote yule hata akiwemo yeye mwenyewe Polepole nitamshinda tu." ameongeza Lema.

Novemba 17, 2019 akiwa mkoani Arusha Katibu wa Itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Humphrey Polepole, alimtaka Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, kutafuta kazi nyingine ya kufanya kwa kile alichoeleza chama hicho kimejipanga kuhakikisha kinapata ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020.