Jumanne , 10th Sep , 2019

Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amedai maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania jana yalikuwa maamuzi ya hofu, kwa kile alichokieleza walifuata vitu vya msingi kwenye kufungua shauri hilo.

Lissu ametoa kauli hiyo baada ya Mahakama kutoa uamuzi wa kuyakataa maombi yake, kwa kile ilichokisema Lissu alipaswa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi ambao ulimpitisha Miraji Mtaturu.

Lissu amesema kuwa "nimewasiliana na Wakili Peter Kibatala kuhusu uamuzi wa Jaji Matupa, huu ndiyo aina ya uamuzi unaotolewa na Mahakama iliyoingiwa na hofu ya watawala, sisi hatukuwa na bado hatuna ugomvi na Tume ya Uchaguzi wala na Miraji Mtaturu."

"Hatukukosea chochote kufungua maombi ya marejeo ya Kimahakama, hoja ya kwamba kutakuwa na mgogoro wa Kikatiba, Wabunge wawili ni hoja isiyokuwa na mantiki au maana yoyote, tulichoomba sisi ni Mahakama Kuu itamke kama uamuzi wa Spika Ndugai ulikuwa sahihi kisheria?" amesema Lissu.

Jana Septemba 9, 2019 Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa maamuzi ya kuyakataa maombi ya Tundu Lissu juu ya kuvuliwa Ubunge na Spika wa Bunge Job Ndugai, na kumpa maelekezo ya kuyafuata.