Jumanne , 29th Sep , 2020

Mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameelezea historia yake na Kijiji cha Nyamongo huku akidai kuwa ametoka mbali na wananchi wa eneo hilo.

Mgombea urais kupitia CHADEMA Tundu Lissu.

Akihutubia katika mkutano wake wa kampeni wilayani Serengeti, Lissu ameeleza jinsi alivyoipambania Nyamongo, tangu akiwa mbunge huku akitaja moja ya eneo alilowapigania ni kwenye suala la madini.

"Mimi nimelala gerezani Tarime kwa sababu ya Nyamongo, nimeshtakiwa Mahakama ya wilaya ya Tarime ni kiwa mbunge kwa sababu ya Nyamongo, nimepigwa na kuchaniwa nguo hadharani nikiwa mbunge mbele ya watu kwa sababu ya Nyamongo,” alisema Lissu.

Aidha, Lissu amewaambia wananchi wa Serengeti kuwa bado hajapokea wito wa maandishi kuhusiana na tatizo lolote kuhusu kampeni zake na kama kuna tatizo ameomba aletewe maandishi yeye mwenyewe kwani ndiye mgombea.

"Hakuna tatizo lolote kama kuna tatizo waniletee maandishi mimi, wasiyapeleke kwenye chama wasiyapeleke nyumbani kwangu, wasiyapeleke kwingine kokote waniletee mimi kwa sababu mimi ndiye mgombea,” alisema Lissu.