Lissu arejea Tanzania, apokelewa na umati wa raia

Jumatatu , 27th Jul , 2020

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA) Bara, Tundu Lissu, hatimaye amewasili nchini Tanzania hii leo Julai 27, 2020, akitokea nchini Ubelgiji alikokuwa akipatiwa matibabu na kupokelewa na mamia ya wafuasi pamoja na viongozi wa chama hicho.

Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, Tundu Lissu, alipowasili Tanzania.

Lissu amewasili majira ya mchana, huku akionekana kuwa ni mtu mwenye furaha kukanyaga tena ardhi na udongo wa Tanzania, baada ya kutokuwepo kwa zaidi ya miaka miwili, hii ni baada ya yeye kushambuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mwaka 2017, wakati akitokea kwenye vikao vya Bunge, kuelekea nyumbani kwake maeneo ya Area D Jijini Dodoma.

Jana Julai 26, 2020, chama chake cha CHADEMA kilieleza kuwa Lissu atakapowasili nchini, siku ya kesho yaani Julai 28, atahudhuria shughuli za utoaji wa heshima za mwisho kwa Taifa kwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.