Alhamisi , 14th Feb , 2019

Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu amefunguka kuwa hakuna ukweli wowote kuwa chama chake kimehusika na shambulio dhidi yake kwani nyumba ile ina ulinzi na walinzi wameajiriwa na serikali.

Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu.

Lissu amesema kuwa kama kuna mwenye uwezo wa kuondoa walinzi lindoni muda wa kazi bila kujua walikuwa wapi na kwanini basi ndio atakuwa amehusika na shambulio hilo.

"Nimekaa eneo lile kwa zaidi ya miaka 7, CCTV Camera zipo na walinzi wapo siku zote sasa Waziri anapokanusha hili atueleze, nini kimetokea na Camera imeng'olewa lini na nani?", amehoji Lissu.

Lissu ameongeza kuwa, "kama Mbowe na CHADEMA wana uwezo wakuondoa Camera na walinzi katika eneo wanaloishi viongozi wa serikali basi watakuwa wamehusika wao, lakini hicho ni kitu ambacho hakiwezekani".

"Yale majengo yanalindwa massa 24 siku 7 za wiki, na hao walionishambulia walinifuata mpaka getini na hao walinzi wanaolinda lile geti siku nashambuliwa hawakuwepo, swali ni Je, nani aliyewaondoa?", ameongeza Lissu.

Jana akizungumza jijini Arusha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema kuwa, “Lissu ndiye mlalamikaji wa kesi, inakuwaje mwenye kesi naye mpaka tuanze kulazimishana ili aje, mwanzoni tulidhani ni mgonjwa akipata nafuu atakuja kwenye kesi yake, tunamshuhudia kapata nafuu kaanza uzembe na uzururaji tunamtaka Lissu arudi nchini".

Lissu anaendelea na ziara zake barani Ulaya ambapo sasa hivi yupo nchini Marekani.